24 Machi 2022 - 16:03
Malengo ya mikutano ya Bennett, Bin Zayed na Al-Sisi huko Misri

Waziri Mkuu wa Israel na Mwanamfalme wa Abu Dhabi wamekutana na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri katika ziara zao nchini humo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Naftali Bennett alisafiri mjini Cairo Jumatatu Machi 21, 2022, na vyanzo vya utawala wa Kizayuni wa Israel na Misri havikutangaza saa na tarehe ya ziara ya hiyo ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni. Ziara ya Bennett nchini Misri ni ya pili katika kipindi cha miezi sita baada ya kukutana na Abdel Fattah al-Sisi huko Sharm el-Sheikh Septemba mwaka jana. Sambamba na safari ya Bennett mjini Cairo, Muhammad bin Zayed, Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi, pia alifanya safari huko Sharm el-Sheikh na kukutana na al-Sisi.

Inasemekana kuwa, mazungumzo ya Vienna kati ya Iran na kundi la 4+1 yalikuwa kiini cha mazungumzo ya pande tatu kati ya Bennett, Bin Zayed na al-Sisi. Mazungumzo ya Vienna yamo katika siku zake za mwisho na ushahidi na taarifa zinaonyesha kuwa, pande husika ziko katika hatua za kufikia makubaliano, suala ambalo haliziridhishi baadhi ya pande hasa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala huo, ukishirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu, unalenga kuzuia uwezekano wa kupatikana mapatano ya nyuklia na kuimarika ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Inaonekana kuwa, suala la kuimarishwa uhusiano kati ya utawala wa Kizayuni na nchi za Kiarabu pia lilikuwa moja ya malengo makuu ya mkutano huo wa pande tatu. Jambo linalozikutanisha pamoja Misri na Imarati ni kwamba nchi zote mbili zina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Wakati huo huo utawala wa Kizayuni pia unakaribisha suala la kuzidishwa uhusiano wake na Misri ikiwa ni miongoni mwa nchi kubwa na muhimu za Kiarabu, na vilevile Imarati ambayo ni miongoni mwa nchi tajiri zaidi za Kiarabu.

Mikutano na mazungumzo hayo ya kidiplomasia, ambayo yameshirikisha Imarati (UAE), pia ina madhumuni na malengo mengine maalumu. Imarati inakusudia kuongeza idadi ya nchi zilizo na uhusiano wa kidiplomasia au kupanua uhusiano wao na utawala haramu wa Israel ili kupunguza mashinikizo ya maoni ya umma katika Ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya nchi hiyo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa, mikutano hii ya kidiplomasia pia ina malengo ya pande mbili. Tovuti ya I-24 imemnukuu Naftali Bennett akisema kuhusu sababu za safari hiyo kwamba: "Tunazungumza juu ya hatua zaidi za kuimarisha makubaliano ya Israeli na Misri,” Televisheni ya al Jazeera ya Qatar pia imeripoti kuwa, mkutano huo ulifanyika baada ya kufikiwa makubaliano mapya kati ya Tel Aviv na Cairo. Makubaliano hayo yanahusu safari za moja kwa moja za ndege kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) hadi Sharm el-Sheikh. Duru za habari nazo zinasema kuwa, kipindi cha sasa kinashuhudia ongezeko la mawasiliano kati ya maafisa wa ujasusi wa Misri na wenzao wa Israel ili kufanyia marekebisho baadhi ya vifungu vya makubaliano ya Camp David.

Kwa upande wake, Imarati pia inajaribu kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Misri na kuwekeza katika sekta ya uchumi ya nchi hiyo. Msemaji wa Rais wa Misri ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuhusu ziara ya Mrithi wa Ufalme Abu Dhabi na mazungumzo yake na al-Sisi kwamba: "Rais amesisitiza hamu ya Misri ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali na Imarati."

Jambo lingine ni kwamba baadhi ya vyanzo vimeeleza kuwa Misri inajaribu kuishawishi Tel Aviv kuwa mpatanishi katika uhusiano kati ya Washington na Riyadh, ambao umedorora tangu Joe Biden aingie madarakani Januari 2021.

Katika uwanja huo, tovuti ya al-Arabi al-Jadeed imeripoti kwamba mazungumzo ya al-Sisi na Bennett yalijikita katika suala la uungaji mkono wa Tel Aviv kwa uhusiano wa Saudia na Marekani.

342/